0
                    ZIARA KENYA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta wamezindua barabara ya Southern By-pass iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi nchini Kenya.

Sherehe ya uzinduzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 28 na inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi imefanyika katika eneo la Karen nje kidogo ya Jiji la Nairobi.

Akizungumza katika sherehe hiyo Rais Magufuli amempongeza Rais Kenyatta na Serikali yake kwa kujenga barabara hiyo ambayo sio tu itawasaidia wananchi wa Kenya bali pia itawasaidia wananchi wa Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.

Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali ya China kupitia benki yake ya Exim ambayo imetoa mkopo wa kujenga barabara hiyo, kwa kuendelea kuziamini nchi za Afrika Mashariki na kuzikopesha mikopo inayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli za maendeleo ya wananchi.



                                  MAJI
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Gerson Lwenge amesema Serikali imeanza mpango wa kujenga mabwawa maalumu.
Lwenge ameyasema hayo leo wakati akizindua mkutano wa Muungano wa Wadhibiti wa Huduma za Maji Kusini na Mashariki ya Afrika (Esawas).
Amesema maji hayo yakivunwa yatatumika katika kilimo cha umwagiliaji na kunywesha mifugo na matumizi mengine makubwa.
                                                MAHAKAMA
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kujenga Mahakama 40 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuongeza ufanisi na kuharakisha hukumu za kesi katika ngazi mbalimbali nchini.


Hayo yamebainishwa mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki Allan Kiula aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na uteuzi wa Mahakimu katika ngazi hiyo.

Waziri Mwakyembe amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Mahakama zinakuwepo kila wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi, kurahisisha usikilizwaji wa kesi pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufuata Mahakama .
Akifafanua mgawanyiko wa Mahakama 40 zinazotarajiwa kujengwa nchini, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itajenga Mahakama Kuu nne, Mahakama za mikoa sita, Mahakama za Wilaya 14 na Mahakama za Mwanzo 16 katika wilaya mbalimbali nchini.
Na, Paulina                                            Chanzo:Michuzi

                                     DIRA
Serikali imeainisha maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2017/2018 kulingana na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema hayo leo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Dkt. Mpango amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na miradi ya kielelezo ya maendeleo ambayo inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni pamoja na miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mchuchuma Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa km 1,251 kwa “Standard Gauge.

Aidha  pamoja na matawi yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa km 379, Isaka hadi Rusumo km 371, Kaliua kupitia Mapanda hadi Karema km 321, Keza hadi Ruvubu km 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati yenye urefu wa km 203.

                                KIMATAIFA                   
Ikulu ya Marekani imeingia katika mgogoro ambao umetikisa kampeni za urais, katika hatua za kufunga kampeni hizo.
Rais Obama amesema hamuamini mkurugenzi wa shirika la upelelezi nchini humo, James Comey,na kuwa anajaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi huo.
Viongozi wa juu wa Democratic wamemkosoa vikali Bwana Comey baada ya shirika la upelelezi wiki iliyopita kusema kuwa lilikuwa likichunguza uwepo wa barua pepe mpya zilizogunduliwa zaweza kumuhusu Bi Clinton.

Mapema uchunguzi wa shirika la upelelezi la Marekani lilisema kuwa watumishi wa barua pepe binafsi ya Bi Clinton walizifuta barua za makosa ya kihalifu za Bi Clinton.
Akiongea mjini Ohio, Bi Clinton amesema kuwa alikuwa na uhakika kwamba shirika hilo la upelelezi lingesema hivyo kwa mara nyingine tena.
                           
                             KIMATAIFA               
Mahakama ya Kimataifa inyoshughulikia kesi za Uhalifu wa kivita ICC imeungwa mkono na nchi nyingi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, siku chache baada ya nchi tatu za Kiafrika kutangaza kujiondoa katika mahakama hiyo.
Hata hivyo Kenya ambayo imechunguzwa na mahakama hiyo, iliipinga vikali na kutilia shaka ikiwa itaweza kudumu muda mrefu. Balozi wa Kenya Tom Amolo hakutangaza iwapo nchi yake pia itajiondoa, lakini alisema inafuatilia mchakato huo kwa makini.
Wengi walipendekeza mazungumzo kati ya mahakama hiyo na nchi za kiafrika ili kushughulikia hofu za nchi za bara hilo, na kuahirisha uamuzi wa Burundi, Afrika Kusini na Gambia kuondoa uanachama wao.
Nchi tatu za kiafrika, Nigeria, Senegal na Tanzania ziliitetea ICC, zikisema ni chombo muhimu katika kupambana na uhalifu mkubwa duniani, yakiwemo mauaji ya kimbari.
ICC imekuwa ikishutumiwa na nchi za kiafrika kulilenga bara lao huku ikifumbia macho uhalifu unaofanywa katika sehemu nyingine za dunia.

                    MICHEZO NA BURUDANI
Yanga wanaamini wako tayari kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Yanga ni wageni lakini Kocha Hans ven der Pluijm amesema wamejiandaa vema wakati leo itakuwa ni siku moja kabla ya pambano.

Yanga waliwasili Mbeya jana na kupokelewa na mashabiki wao kwa wingi ambao walionyesha kuwa wanahitaji furaha kwa wao kushinda, kesho.


Baada ya mechi hiyo, Yanga wataendelea kubaki mjini Mbeya kuisubiri Prisons katika mechi itakayopigwa kwenye uwanja huohuo, Jumamosi.


Kabla ya mechi ya kesho, Yanga imeonekana ni moto wa kuotea mbali baada ya kushinda mechi tatu kwa jumla ya mabao 13.
              =======      =======   =======
SHIRIKISHO la mpira wa miguu  nchini TFF,limepokea mwaliko kutoka chama cha mpira wa miguu nchini Zimbabwe juu ya chama hicho kuhitaji kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na timu ya Tanzania Taifa Stars.

Afisa habari wa TFF,Alfred Lucas amesema kwamba mara baada ya kupokea baraua hiyo shirikisho la soka hapa nchini limeridhia swala hilo na kwa sasa wakati wowote kuanzia sasa kocha mkuu wa timu ya Taifa Charles Boniphace Mkwasa ataanza program kwa ajili ya mechi hiyo inayotaraji kupigwa siku ya tarehe 13 mwezi huu.

 Kocha Mkwasa anatarajiwa kutangaza kikosi hivi karibuni na wataingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ambayo ni muhimu kwao kwa ajili ya kupanda viwango vya FIFA.
                  =====   ======    ======



Post a Comment

 
Top