0
       
TAARIFA YA HABARI KUTOKA RADIO SENGEREMA.

ZAHANATI.
Zahanati ya kijiji cha Balatogwa iliyopo kata ya Mwabaluhi Wilayani Sengerema  inakabiliwa na  ukosefu wa vifaa tiba ikiwemo hadubini, hali ambayo   inawalazimu wakazi wa kijiji hicho pindi wanapohitaji kupatiwa vipimo kutembea umbali wa kilomita saba kwenda  Hospitali Teule ya  Wilaya  ya Sengerema kufuata vipimo hivyo.

Katika mahojiano na Radio Sengerema baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema kuwa hali hiyo inawapa usumbufu mkubwa na kwamba  licha ya kuwepo zahanati hiyo katika kijiji chao , hawanufaiki na    matunda yake kutokana na kukosa vifaa tiba.
Evanjelista Mbuke  ni muuguzi wa zahanati ya kijiji cha  Balatogwa amesema   pindi inapotokea watu wengi wanahitaji vipimo hukosa vipimo kwa sababau ya changamoto ya vifaa hivyo. 
Clip Muuguzi Balatogwa…..
Kwa upande wake  Mganga Mkuu wa Zahanati hiyo  Timoth  Mashauri amekiri kuwepo kwa ukosefu wa vifaa tiba katika zahanati hiyo na kuiomba serikali kufanya jitihada za makusudu kupeleka vifaa hivyo ili kuwaondolea usumbufu wanaoupata wananchi.

Na,  Mhariri  Twimanye    Chanzo       Mahojiano.

UKOSEFU WA SHULE
Kata ya Ibisabageni wilayani Sengerema inakabiliwa    na   ukosefu wa shule ya    sekondari  , hali inayopelekea wanafunzi wa kata hiyo  kutembea  umbali mrefu  kwenda   kusoma kwenye shule za kata jirani.
Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa kata ya Ibisabageni  Mh, Jumanne Masunga   ambapo amesema  wamekwishaanza jitahada za ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kwenda shule za kata jirani.
Hata hivyo Masunga   amewaomba  wenyeviti wa vitongoji vyote vilivyopo kwenye kata yake wachangishe michango kwa wananchi ili zoezi la ujenzi liweze kukamilika haraka iwezekanavyo ili kuwarahisishia wanafunzi mazingira ya usomaji.

Na Veronica /Mahariri  Twimanye          Chanzo Mahojiano.




KUPANDA MITI
Mkuu wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu Tano Mwela amewaagiza wataalamu  wa mashamba na watendaji wa mashamba wilayani humo kuwa na orodha maalumu ya wakulima wote wa maeneo yao na kuhakikisha kila familia inalima hekali nne, ikiwa hekali mbili ni za chakula na mbili   za mazao ya biashara.
Ametoa agizo hilo wakati akizindua kampeni ya upandaji miti  wilayani humo inayojulikana kwa jina la mti wangu ambapo amewahimiza wakazi hao kupanda miti kwa wingi   ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea.
Miti aina mbalimbali imezinduliwa wilayani humo ambapo miti zaidi ya milioni 2 inatarajiwa kupandwa kwa kila mwaka ili kurudisha uoto wa asili ambao ulikuwa umeanza kupotea kutokana na ukataji wa miti ovyo.
Aidha wilaya hiyo imepanga kupanda miti ya matunda 200 pamoja na miti mingine inayowawezesha kupata mbao na kivuli.
Na Veronica/Mhariri   Twimanye    Chanzo     TBC.



 TUKIO
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania Mwigulu Nchemba ameliagiza jeshi la polisi kuwasaka na kuwakamata   walimu watatu wa mafunzo ambao wanadaiwa kumpiga mwanafunzi  shuleni  Mkoani Mbeya .
Video ambayo inadai kuonyesha tukio la mwanafunzi huyo akipigwa imesambaa   mtandaoni Tanzania na Kenya.
Kupitia taarifa, Bw Nchemba, amesema uchunguzi wa awali unaonesha tukio hilo lilitokea katika shule ya upili ya Mbeya    Septemba. 28 mwaka huu ambapo  Walimu hao walikuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo.
Anasema mwalimu mmoja alikuwa amewapa wanafunzi zoezi la Kingereza lakini baadhi ya wanafunzi wakasusia kulifanya na ndipo mwalimu mmoja  alimpiga kofi kijana na kijana akahoji kwanini anampiga ndipo  walimu wakamchukua na kumpeleka  chumba cha walimu     na kuanza kumpiga. 
Tangu kutokea  kisa hicho, inaarifiwa  kwamba mwanafunzi huyo hajaonekana shuleni tena.


KIMATAIFA.
Watu  sita   wameuawa  baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Taarifa zinasema washambuliaji hao wamevamia eneo lenye nyumba za makazi Bulla usiku wa manane.
Gavana wa jimbo la Mandera Ali Roba ameandika kwenye  mitandao ya kijamii  kwamba watu 6 wameuawa na mmoja kujeruhiwa.
Amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye ploti hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.
Kituo kimoja cha redio kinachohusishwa na kundi la al-Shabab kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo.
 Gazeti la Standard nalo linasema walioshambuliwa walirusha guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa al-Shabaab kutoka Somalia.
Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kundi la al-Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio nchini Kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka wa 2013.


MWISHO WA TAARIFA YA HABARI

Post a Comment

 
Top