0
                      
SHERIA MKONONI
Mtu mmoja mkazi wa Nyambogo kata ya Shiloleli mkoani Geita  ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kile kilichodaiwa kuiba  kuku kijijini hapo.

Baadhi ya wananchi wamesema kuwa wamefikia hatua hiyo ya kujichukulia sheria mkononi kutokana na  marehemu huyo kukithili kutenda vitendo vya wizi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mwenyekiti wa mtaa huo  Bw. Magulutatu  Juma amemtaja mtu aliyeuawa kuwa ni Simon Phillipo mwenye umri wa miaka 50.

Hata hivyo Bw. Juma amesema kuwa jeshi la polisi mkoani Geita limefika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata wananchi watano ili kusaidia upelezi  wa tukio hilo.


                             KUSIMAMISHWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi.

Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo  wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng'apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.

Mhandisi huyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila  kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.

                                 NEC


Tume Ya Taifa Ya Uchaguzi (Nec) inaendelea kutekeleza mkakati Wa Kutoa Elimu Ya Mpiga Kura Kwa Wananchi Ili Kuimarisha Demokrasia Nchini.

Mwenyekiti Wa Tume Hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametoa Wito Kwa Wananchi Kuendelean Kutoa Ushirikiano Wao Kwa NEC Ili Kufanikisha Mkakati Huo
Kwa Upande Wake Mkurugenzi Wa Uchaguzi Wa Tume Ya Taifa Ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani amewataka Wananchi Kuhakikisha Elimu Ya Mpiga Kura Inawafikia na kuielewa ili waweze kutambua demokrasia.

Mkakati Wa Kutoa Elimu Ya Mpiga Kura Ni Utekelezaji Wa Kifungu Cha 4 (C) Cha Sheria Ya Uchaguzi Ya Mwaka 1985 Inayoitaka Tume Ya Taifa Ya Uchaguzi Kutoa Elimu Hiyo, Kusimamia Na Kuratibu Asasi Na Taasisi Zinazotaka Kutoa Elimu Ya Mpiga Kura.
                             MKATABA.

Ubalozi wa Norway nchini umesaini mkataba wenye thamani ya Tsh. Bilioni 10.6 na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Mpango wa Misaada ya Maendeleo (UNDAP 2) kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi waliopo hapa  nchini.


Akizungumza katika hafla ya utilianaji saini mkataba huo, Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad amesema pesa ambazo wamezitoa zinalenga zaidi kuwasaidia wakimbizi waliopo mkoani Kigoma ili waweze kuwa na shughuli za kuwasaidia na hasa kwa wanawake na watoto.


Nae Mratibu Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez amesema ni jambo zuri kuona Norway inaendeleza ushirikiano na Tanzania na wao wamejipanga kuhakikisha wakimbizi wanaokusudiwa kunufaika na pesa hizo zinawafikia na kufanya kazi ambayo zimepangiwa kufanyika.

                                    UTALII
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema tabia ya udokozi ni miongoni mwa sababu ambazo zinazowafanya wenye hoteli wapende kuajiri wageni badala ya watanzania.
Mwandishi wetu SARAH CHARLES anataarifa zaidi.
Akizungumza na wafanyakazi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Maghembe amesema kazi za hoteli zinahitaji watu waaminifu na wanaojituma.
Profesa Maghembe ametoa wito kwa uongozi wa chuo hicho kufundisha uaminifu  katika kazi ili wageni waweze kukaa kwa amani.
                                                      KIMATAIFA                   
Biashara zimefungwa Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na hakuna magari barabarani kufuatia wito wa upinzani kuwa watu wakae ndani katika kushinikiza uchaguzi mkuu nchini ufanyike Novemba na Rais Kabila ajiuzulu.
Mwandishi wa BBC aliyeko mjini Kinshasa anasema vikosi vya usalama vimeizingira nyumba ya mpinzani mkuu wa rais Kabila, Etienne Tshisekedi, ambaye ndiye anaongoza wito wa uchaguzi ufanyike Novemba mwaka huu.
Chama chake kimeonya kuwa rais Kabila atakuwa anatekeleza 'uhaini wa hali ya juu' iwapo uchaguzi utacheleweshwa.
Katiba inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu, na upinzani unatuhumu kuwa serikali inataka kuchelewesha uhaguzi huo ili Kabila asalie madarakani.
Chama tawala na kimoja cha upinzani vimependekeza kuchelewesha uchaguzi wa urais hadi  mwezi Aprili 2018.

Watu kadhaa wameuawa mjini  Kinshasa mwezi uliopita katika maandamano ya kumtaka rais Kabila aondoke madarakani
                  
                           KIMATAIFA 
                 
Ethiopia imedhibiti usafiri wa wanadiplomasia wa kigeni na kupiga marufuku mikutano na upinzani ulioko nje ya nchi kama sehemu ya hali ya hatari iliotangazwa nchini humo.

Wanadiplomasia hawaruhusiwi tena kusafiri zaidi ya kilomita 40 nje ya mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Vikwazo hivyo vipya vinahusisha pia kile kinachotajwa kuwa "ukanda mwekundu" wa maili 30 kwenye mipaka ya nchi hiyo, ambapo ni haramu kubeba silaha, na pia amri ya masaa 12 ya kutotembea usiku katika maeneo ya viwanda na karibu na majengo ya serikali.


Hatua hizo zimeanzishwa kufuatia wimbi la maandamano ya kuipinga serikali.



                 MICHEZO NA BURUDANI
Mwanasoka wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji amesema kwamba kuingizwa kwenye kinyang'aniyo cha tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika ni heshima kuu kwa nchi yake.
Samatta, amesema amefurahi juu ya uteuzi huo, kwani anajiona anaendelea kuiwakilisha vyema nchi yake katika soka.
Mwanasoka Bora wa Afrika pamoja na kipa Mganda, Dennis Onyango anayechezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kiungo Mkenya, Victor Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur ya England.
Orodha hiyo ina Waalgeria watatu; mshambuliaji wa mabingwa wa England, Riyad Mahrez, Islam Slimani wa Leicester City na El Arabi Hillel Soudani wa Dinamo Zagreb.

                   =======      =======   =======
Bondia wa Tanzania Dulla Mbabe Oktoba 28 anatarajia kupambana na Bondia Chengbo Zheng kutoka Taifa la China Pambano la WBO katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa mwandaaji wa pambano hilo Jay Msangi, mshindi wa pambano hilo atajinyakulia Mkanda wa ubingwa, huku pia kukiwa na mapambano mengine mengi ya utangulizi ambayo yatawakutanisha mabondia kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.
Jay Msangi amesema kwa sasa wataandaa mapambano mengi ya kimataifa kwa mabondia wa Tanzania kwa lengo la kuwandaa kufuzu mashindano ya Olimpiki nchini Japan.

                              BIASHARA       
KAMPUNI ya Uwekezaji ya TCCIA imejipanga kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, ili kuchangia kukuza uchumi wa taifa na ajira.

Akifungua mkutano mkuu wa 11 wa kampuni hiyo Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Aloys Mwamanga, amesema wamejipanga kuanzisha viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo.

Amesema kampuni inaunga mkono kwa dhati dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika sekta ya viwanda na hasa viwanda vya kusindika mazao.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kampuni imepanga kuwekeza pia katika dhamana za Serikali, benki, uanzishaji wa taasisi za fedha zinazohusika na mitaji midogo, ujenzi wa jengo la ofisi na maghala ya kuhifadhi bidhaa.

                                 BIASHARA                 

Wito umetolewa kwa jamii ili waweze kuwa na maisha bora wawe na shughuli za halali za kufanya zitakazo waingizia kipato,ili wasiwe tegemezi katika familia zao na jamii kwa ujumla. 

Kauli hiyo imetolewa na Jaggy Singh ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa ushirika ( FGBMFI) wa Kimataifa wa wafanyabiashara Wakristo,ambapo amewataka watu kufanya shughuli zao katika misingi iliyo halali ,katika uadilifu na waepuke udanganyifu.


Sigh amesisitiza kuwa lengo kuu la mkutano ni kuwaleta wafayabiashara pamoja, kubadilishana mawazo na changamoto wanazopitia,kuonyesha umuhimu wa kuishi maisha ya uhalisia na kufanya kazi kwa bidii zaidi,ambapo amewataka kuepuka udanganyifu kwa kutokulipa kodi ,wafuate utaratibu na sheria za nchi. 



Post a Comment

 
Top