0
 TAARIFA YA HABARIKUTOKA RADIO SENGEREMA FM
HUKUMU
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu Ally Rashid  , kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 25, katika Mtaa wa Kotazi, Manispaa ya Mpanda..

Hukumu hiyo imetolewa    na  Hakimu wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pasipo kutia shaka, ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Jamila Mziray.

Awali Mwendesha Mashtaka Mziray alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 17, mwaka huu, saa 2:00 usiku katika makaburi ya Kashaulili yaliyoko katika Mtaa wa Kotazi, Manispaa ya Mpanda.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimfuata msichana huyo ambaye alikuwa ameibiwa vitu vyake vya ndani ya nyumba  na kuwa ana uwezo wa kumsaidia kuvipata vitu vyote alivyoibiwa.

Mziray amedai kuwa baada ya msichana huyo kuahidiwa na mshtakiwa kuwa vitu vyake alivyoibiwa vitapatikana alimlipa mshtakiwa Shilingi  elfu thelathini    ili akamwoneshe vitu vyake alivyoibiwa.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku hiyo ya tukio mshtakiwa alimpigia simu msichana huyo saa 2:00 usiku akimtaka waonane ili akamwonesha vitu vyake vilivyoibiwa.

Mziray ameeleza mshtakiwa alikwenda nyumbani kwa msichana huyo na wakaongozana hadi kwenye makaburi ya Kashaulili ambako alidai ndiko vilipo vitu vilivyoibwa lakini ghafla mshtakiwa alimpiga ngwala msichana huyo na kumbaka  na kumlawiti huku akimtishia maisha iwapo akijaribu kupiga kelele.
TANESCO
Shirika  la Umeme Nchini Tanzania, TANESCO, limewatahadharisha wananchi mkoani Kagera kutogusa  nyaya za umeme kwenye nyumba zilizoanguka au kupata athari kubwa kutokana na tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera wakati wafanyakazi wa Shirika hilo wakiendelea na zoezi la kuondoa nyaya hizo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba,   wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali  mstaafu Salum Kijuu,   ili kumpa pole kutokana na maafa haayo.
Sambamba na wito huo, Mkurugenzi huyo pia amemuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa upatikanaji wa umeme mkoani humo utakuwepo bila shaka yoyote isipokuwa   kwenye maeneo ambayo nyumba zimeathirika vibaya ili kuepusha athari zozote zinazoweza kutokea kutokana na kuguswa kwa nyaya hizo.


KIBAHA
Wananchi   Mjini    Kibaha   wamemuua mtu mmoja  aliyefahamika kwa majina ya Michael Wiliam maarufu kama Michael Dada wakimtuhumu kuwateka watoto wa kike wawili ambao ni wanafunzi kwa lengo la kuwabaka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha, mkoani Pwani na Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi  wananchi hao wenye hasira walimshambulia mtu huyo sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia kifo.
Amesema mtoto wa kwanza aliyehusika katika utekaji nyara huo ana umri wa miaka 11 akiwa anasoma katika Shule ya Msingi Kibaha na wa pili ana umri wa miaka sita akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Chekechea ya Mama Kawili, wote wakiwa wanaishi na wazazi wao eneo la Picha ya Ndege.
Kamanda   Mshongi ,  amesema kuwa watoto hao walikubali na kuanza kuongozana naye lakini wakiwa njiani ghafla lilitokea gari aina ya Toyota Noah lenye rangi nyeusi ambalo namba zake hazikuweza kufahamika mara moja, na kusimama walipo watoto hao na baadaye walishuka watu waliofunika   sura zao kuwabeba watoto hao na kuwaingiza katika gari huku gari hilo likiondolewa kwa kasi kuelekea upande lilipo pori la Shirika la Elimu Kibaha karibu na Shule ya Sekondari ya Tumbi.
Hata hivyo   Kamanda   Mshongi    amebainisha kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa Wiliam alikuwa mhalifu mzoefu na alikuwa akifanya matukio mara kwa mara ikiwemo ubakaji na wizi wa mifugo.

MAGEREZA
Mkuu wa magereza Jenerali John Minja  amezuia kupandishwa vyeo kwa askari kadhaa wa jeshi la magereza  ambao wamehitimu mafunzo katika chuo cha Fubila kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya baada ya kubaini kuwa na kasoro ikiwa ni pamoja na utoro na kushindwa kufuatilia kikamilifu mafunzo ya uongozi wa daraja la kwanza.
Jenerali Minja ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya uongozi wa  daraja la  kwanza  kozi namba 22  kwa wahitimu waliofika 80 katika chuo cha Fubila.
Mkuu wa  jeshi la magereza nchini jenerali Jihn Minja ametangaza rasmi utaratibu mpya wa upandishwaji wa vyeo kwa askari wa jeshi hilo na hii ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya askari wamekuwa wakitoroka mafunzo.
Kwa upande wake katibu mkuu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi meja Jenerali Polojest  Lwegasila ametoa maelekezo ya kuheshimu misingi ya kazi.
Na Veronica /Mhariri  Twimanye            Chanzo TBC


KIMATAIFA.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa wakereketwa 16 wa demokrasia  wametiwa mbaroni katika Jamhuri ya  Demokrasia ya Congo.
Umoja wa Mataifa umehimiza taifa hilo kuheshimu haki za kimsingi za kibinadamu nchini humo.
Umoja wa Mataifa pia unasema kuwa watu wengine 85 wametiwa mbaroni katika mji mkuu wa Lubumbashi, baada ya makabiliano makali kati ya maafisa wa usalama na wafuasi wa vyama vya upinzani siku ya   Ijumaa.

Uchaguzi unatarajiwa mnamo Novemba, lakini tume ya uchaguzi inasema kuwa uchaguzi huo utacheleweshwa.

Upande wa upinzani unamlaumu rais Joseph Kabila, ambaye haruhusiwi kikatiba kugombea kiti hicho tena, kwa kuchelewesha uchaguzi huo makusudi.





KIMATAIFA.
Marekani imesema inasikitika juu ya shambulio lililoongozwa na ndege zake za kivita ambapo, bila kukusudia zimelipua kambi za wanajeshi wa Syria.
Wakati huohuo Marekani imekosoa Urusi kwa kuitisha mkutano maalumu wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ikisema hatua hiyo ya Urusi kutaka kuwakosoa Marekani bila sababu maalumu.
Urusi  inasema kuwa wanajeshi 60 wa Syria waliuawa katika shambulio hilo la Kaskazini Mashariki mwa Syria.
Makao Makuu ya Kijeshi yanasema kuwa ndege hizo zilidhania kuwa zilikuwa zikishambulia kambi za makundi ya Islamic State, ambazo Marekani inasema zilikuwa zikitafuta kwa siku kadhaa.
Lakini Urusi inasema kuwa Marekani walikuwa na lengo la kuwasaidia wanachama wa Islamic State na kuongezea kuwa mapatano yake na Marekani kuhusiana na usitishaji wa mapigano umehatarishwa.
Hakuna habari za kuthibitisha idadi ya watu waliouawa.

NA HUO NDIO MWISHO WA TAARIFA YA HABARI KUTOKA RADIO SENGEREMA FM.



Post a Comment

 
Top